Saturday, November 21, 2009

Wanawake watembea kilometa 30 kudai mbolea ya ruzuku

Kilimo Kwanza inavyoendelea kuzua majambo!

Wanawake 26 wakazi wa kijiji cha Ndolezi wilayani Mbozi mkoani Mbeya jana waliandamana umbali wa kilometa 30 kwa miguu hadi ofisi ya mkuu wa wilaya ya Mbozi kupeleka madai ya kunyimwa mbolea ya ruzuku.

Kiongozi wa wanawake hao Mary Anyangalile ameliambia gazeti hili kuwa Afisa Mtendaji wa kijiji chao amewanyima mbolea na kuwapa wanaume kwa madai kuwa wanawake hawastahili kupewa mbolea hizo. Aidha aliongeza kudai kuwa mgawo wa mbolea hizo unaotolewa kwa upendeleo umewapa vijana wadogo ambao hawana nyumba (hawajaoa) na hivyo kuwafanya wao waamini kuwa kuna mazingira ya rushwa.

Linas Hebron, mmoja wa wanawake hao alieleza kuwa kaya nyingine zimepewa hadi mifuko 4 ya mbolea ili hali wao hawakupata na kwamba hawastahili kupata ndiyo maana wanataka kumwona mkuu wa wilaya awasaidie watambuliwe na kupewa mbolea hizo.

Walalamikaji hao ambao waliandikiwa barua na diwani wa kata ya Mlangali Juma Mnkondya ya kupeleka kwa mkuu wa wilaya hawakufanikiwa kumwona kwa kuwa ilikuwa Jumamosi siku ambayo ni ya mapumziko na hivyo barua yao kupokelewa na afisa tawala aliyejulikana kwa jina moja la Kikosa.

Afisa Mtendaji wa kijiji cha Ndolezi Elia Kalinga alipohojiwa juu ya malalamiko hayo ya wanawake alidai kuwa yeye anawapa wanaume kwa kuwa ndiyo wakuu wa kaya na iwapo wanawake wayo mashamba yao hana mwongozo wa kuwapa mbolea hizo.

Mkuu wa wilaya ya Mbozi Gabrieli Kimolo aliwaambia waandishi wa habari mwishoni mwa wiki kuwa wakulima wana uelewa mdogo juu ya suala la mbolea za ruzuku na hivyo kujiona kuwa wote wanastahili kupata mbolea hizo na ndiyo sababu ya kuwepo kwa migogoro inayoendelea hivi sasa wilayani hapa.

Uchunguzi wangu umebaini kuwepo kwa njama za makusudi za baadhi ya watendaji wa vijiji kujinufaisha kwa kuhodhi baadhi ya vocha za pembejeo na kuziuza kwa mawakala wa usambazaji wa pembejeo. Zoezi la ugawaji wa pembejeo za ruzuku umeingia dosari baada ya kubainika kuibiwa vocha za sh milioni 86 katika ofisi ya kilimo ya wilaya ambapo watuhumiwa wameshafikishwa mahakani.

Uchunguzi zaidi unaonesha njama nyingine za baadhi ya wahusika kuwazunguka viongozi wa vijiji na kuwasainisha hati za mapokezi ya vocha kwa idadi isiyolingana na mapokezi halisi na hivyo kuwatia kitanzini watendaji hao iwapo serikali itafuatilia na kuhakiki mapokezi hayo.
mwisho

Thursday, November 19, 2009

Watumishi watano wa Halmashauri ya Mbozi Kotini kwa wizi wa Vocha za ruzuku ya pembejeo

Watumishi watano wa halmashauri ya wilaya ya Mbozi wamepandishwa kizimbani kujitu tuhuma za wizi wa vocha za pembejeo zenye thamani ya shilingi milioni 86.

Watumishi hao ni Joseph Mbogela (59) afisa kilimo, Asante Ndimbo (46) afisa kilimo na Tekla Luoga (54), wengine ni Maiko Mwashiuya (45) dereva, Goodluck Mbazu (33) dereva na Richard Mnkondya (41) mfanyabiashara aliyepatikana na vocha mali ya wizi zenye thamani ya shilingi milioni 25.

Watuhumiwa wote ambao walishitakiwa mbele ya hakimu wa mahakama ya wilaya Nyasige Kajanja wamekana mashitaka yaliyosomwa dhidi yao na mwendesha mashitaka wa polisi Charles Makunja.

Kesi itatajwa tena Disemba 5, washitakiwa wamepewa dhamana ya maneno ya shilingi milioni 5.

Monday, April 20, 2009

MZEE CHILO AKIWA JIJINI MBEYA


Mzee Chilo akiwa jijini Mbeya akipika filamu mpya matata na tishio ambayo itakuwa madukani hivi karibuni.

Mzee Chilo alivuma sana katika mchezo maarufu wa Jumba la Dhahabu

VIONGOZI WA MAALBINO MBOZI




Maalbino (viongozi) wamelivalia njuga suala la mwenzao aliyetishiwa wiki mbili na mtuhumiwa ambaye hadi sasa yuko uraiani.


Sydney Mwamlima ambaye ni katibu wa Chama cha Maalbino amedhamiria kulifikisha suala hilo kwa mkuu wa polisi mkoani hapa ili kuona anatakeleza maagizo ya serikali kuwalinda.


JESHI LA POLISI NA ALBINO



Wadau hapo juu ni mkuu wa kituo cha polisi mjini Tunduma Ally Wendo akimtaka albino Judith Silwimba kumpa maelezo ya kina juu ya uwepo wa mtuhumiwa aliyemtishia kumuua hapo kijijini Chipaka.


mazungumzo hayo yalizua ubishi kati ya mume wa mlemavu huyo na polisi akidai kuwa ameshakwenda polisi zaidi ya mara tatu lakini hawajamsikiliza na kwamba mtuhumiwa bado yuko huru mitaani.


hapo polisi kazi kwenu

Saturday, April 18, 2009

HOFU KWA MAALBINO

Wadau ni muda mrefu sikuwepo hewani tuungane tena.

Judith Msongole mlemavu wa ngozi (Albino) wa kijiji cha Chipaka wilayani Mbozi anaishi kwa hofu ya kuuliwa! jamani hapo sasa ni mambo!

Jamani uungwana uko wapi? Maisha ya albino yanapokuwa hatarini na hasa watu wanapojitokeza kuwatisha wazi wazi wakiwa na nia ya kuwadhuru na kupata viungo vyao. Sasa mama huyo anaishi kwa hofu, polisi nao wamechelewa kuchukua hatua za kumkamata mtuhumiwa sasa mabishano ni kati ya polisi na mume wa mlalamikaji.

Mkuu wa kituo anadai mlalamikaji hajaenda kumwona ilihali mume wa mlalamikaji anadai kwenda zaidi ya mara tatu polisi lakini wanajibiwa visivyo.

Viongozi chukueni hatua za kukomesha mauaji hayo.

Jakaya Kikwete chukua hatua zile alizochukua Mwalimu Nyerere kukomesha mauaji yaliyokuwa yanatokea Tukuyu hasa Ikuti kwa imani za kishirikina miaka ya sabini. Mbinu ile itasaidia, wachawi wote maarufu kama Manyafu walipitiwa na operesheni ile ambayo iliwahamishia Mafia na kuwekewa stop wasirudi mkoani Mbeya.

Hatuwezi kukuelekeza, bado unao maafisa walioshiriki operesheni ile tafadhali uwatumie japo kwa kiasi. Tuone waganga hao wakifanyia uganga huko uhamishoni ikiwezekana ni kuwakusanya pote walipo.
Pamoja na agizo la Waziri Mkuu Mh. Pinda kufuta leseni za waganga wa jadi bado waganga wanaendelea kutoa huduma kwa wateja huku wakiweka mabango yao barabarani hadharani.

Shiriki hapo ulipo kutokomeza mauaji ya albino.

Saturday, February 28, 2009

VIJANA WENYE HASIRA WAIPIGA MAWE NYUMBA YA MWENYEKITI WA HALMASHAURI

Na Kenneth Mwazembe
Tunduma

Kundi la vijana wenye hasira kali zilizochochewa na mkuu wa kituo cha polisi mjini Tunduma A.S. Wendo wamevamia nyumba ya diwani wa kata ya Tunduma na ambaye pia ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mbozi Aden Mwakyonde na kuvunja vioo 83 vya madirisha 14 na kuwajeruhi mgambo wanne.

Chanzo cha ghasia hizo ni kukamatwa kwa baiskeli za vijana hao zilizokuwa zikitumika kuvusha mahindi na mchele mpakani mwa Tanzania na Zambia kwa madai kuwa ni operesheni usafi wa mji.

Vijana hao wamesema kuwa polisi walianza ukamataji wa baiskeli hizo usiku wa Februari 26 na kuendelea 27 ambapo vijana hao wamedai kuwa wamedaiwa fedha (RUSHWA) ili kukomboa baiskeli hizo.

Katika kukabiliana na kitendo hicho ambacho wamekiita unyanyasaji unaofanywa na jeshi hilo vijana hao waliandamana kuelekea kituo cha polisi ili kuishinikiza polisi kuwarejeshea baiskeli zao ambapo mkuu wa kituo aliwaambia waende kuchukua baiskeli hizo kwa diwani wao.

Kauli hiyo ndiyo iliyowafanya wao kurusha mawe kituoni hapo na baadaye kwenda nyumbani kwa diwani wao na kuharibu madirisha yote na kuipiga mawe nyumba hiyo.

Akizungumza na gazeti hili Aden Mwakyonde alieleza kuwa alipigiwa simu na mwenyekiti wa kamati ya ulinzi shirikishi ya mjini hapa kuwa kuna maandamano makubwa ya vijana wenye hasira wakienda nyumbani kwake hali iliyomfanya awapigie askari polisi.

“Nimepiga simu kwa OCS ili atume askari kuzuia madhara ambayo yangeweza kutokea lakini hakufanya hivyo, alidai hana gari, mke wangu amempelekea magari mawili akadai hawawezi kutumia salon wanataka gari la wazi hata alipopelekewa gari la wazi akasema ni chakavu kasha akaondoka kwenda mjini Vwawa” alilalama Mwakyonde.

“Nimewaomba polisi wawape vijana hao baiskeli zao ili kuepusha shari ambayo ingeweza kutokea lakini polisi hawakufanya hivyo na hivyo kunisababishia hasara hii ”aliongeza Mwakyonde akielekeza lawama zote kwa jeshi la polisi.

Mwenyekiti huyo aliyekua akihudhuria kikao cha kamati ya uchumi na mipango alilazimika kuacha kikao na kukimbilia nyumbani kwake akiwabeba mkuu wa polisi wilayani hapa Stephen Mtengeth na timu yake lakini alipofika na kuona nyumba imeharibiwa aliwajia juu na kuwafukuza OCD na timu yake ya watu wane.

Hatua hiyo na ambayo imewaudhi polisi hao imelalamikiwa vikali kutolewa na kiongozi kama yeye wakidai angetumia busara.

Mkuu wa kituo cha polisi cha Tunduma aliyejitaja kwa jina moja la A. S. Wendo alipohojiwa juu ya yeye kuwa chanzo cha ghasia hizo alikanusha na kudai kuwa yeye amewatuliza wakakataa na hivyo kumfanya aende wilayani kuomba msaada wa askari wengine.

“Niliamuru kupigwa kwa mabomu ya machozi ili kukinusuru kituo baada ya vijana hao kutaka kukivamia” anaongeza Wendo.

Mamlaka ya mji mdogo wa Tunduma inafanya operesheni ya kusafisha mji kwa kuondoa uchafu katika mifereji na vibanda vya wafanyabiashara ndogondogo ambayo ilianza juzi ikahamia na kukamata baiskeli hali iliyozusha machafuko yaliyosababisha wanamgambo wa halmashauri wane kujeruhiwa na mmoja kulazwa katika hospitali ya wilaya ya Mbozi mjini Vwawa.

Mgambo waliojeruhiwa ni John Mwakalinga ambaye amelazwa katika hospitali ya Vwawa na Andrew Sing’ambi aliyetibiwa na kuondoka na wengine wawili ambao hawakuweza kupatikana majina yao .

Muuguzi katika wodi la majeruhi Ester Nyondo ameeleza kuwa hali ya mgonjwa huyo inaendelea vizuri.

Hili ni tukio la tatu tangu mwaka 2006 ambapo ghasia za mpakani zilizuka kufuatia kifo cha Lukas Msuya kuuawa katika mahabusu za Zambia lile la mgomo wa mawakala wa usafirishaji (Clearing & Forwarding) ambapo katika ghasia hizo kulitokea uharibifu wa mali na majeruhi.

Mkuu wa wilaya ya Mbozi Halima Kihemba alipohojiwa juu ya matukio hayo alikiri kupewa taarifa muda mchache uliopita na kwamba kwa wakati huo alikuwa safarini Tukuyu kwenye kikao.